Jumanne, 24 Aprili 2018

ACT yakomalia Tillioni 1.5 yarejea na hoja tano za ufafanuzi.

ad300
Advertisement
Serikali Iseme Ilipopeleka 1.5 Trilioni za Watanzania, Kuisingizia Zanzibar ni Uongo na Kutudharau Watanzania.
-Hoja 5 za Ufafanuzi wa ACT Wazalendo Dhidi ya kile lilichotajwa kama  Uongo wa Makusanyo ya 203.9 Bilioni ya SMT kwa niaba ya SMZ.
Aprili 20, Serikali ilitoa kauli bungeni, kupitia Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, juu ya shilingi 1.5 trilioni, zisizojulikana matumizi yake kwa mujibu wa ripoti ya UCAG ykwa mwaka wa fedha wa 2016/17. Katika majibu hayo, kuna hoja ya shilingi 203.9 bilioni, ambazo Serikali ya Muungano (SMT) imedai ni mapato ya kodi yaliyokusanywa kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).
ACT Wazalendo tumepitia nyaraka za ukaguzi, kimahesabu na za kibajeti za Serikali zote mbili, SMT na SMZ, ili kujiridhisha na taarifa hizo. Baada ya uchambuzi wa nyaraka hizo tumegundua Serikali kwa makusudi imeendeleza upotoshaji bungeni juu ya zilipo shilingi 1.5 trilioni. Hoja zao zote 3 tunayo majibu ya kuzivunja. Kwa kuanzia, leo tutajibu hoja juu ya shilingi 203.9 bilioni za Zanzibar. Tunazo hoja tano (5) zifuatazo:
1. Bajeti ya Zanzibar na Vyanzo Vyake
Bajeti ya Zanzibar ya mwaka 2016/17 ilikuwa ni shilingi 841.5 bilioni, shilingi 482.4 bilioni kutoka katika vyanzo vya ndani, shilingi 324.8 bilioni mapato ya nje (ruzuku - 93.3b, na mikopo - 231.5b), pamoja na 34.3 bilioni mkopo wa ndani.
Mchanganuo wa Makusanyo ya fedha za ndani ni kama ifuatavyo; Bodi ya Mapato Zanzibar, ZRB (237.4b), TRA Zanzibar (188.8), Mapato ya Mawizara (26.4b), PAYE kwa watumishi SMT (21b), Gawio la faida kutoka BOT (4b), na Gawio la faida kutoka mashirika ya SMZ (4.8b). Maelezo haya yako kwenye hotuba ya Bajeti Kuu ya Zanzibar, 2016/17 iliyotolewa na Waziri wa Fedha wa Zanzibar kwenye Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BLW) wakati akiwasilisha bajeti husika.
2. Makusanyo na Matumizi ya SMZ Mpaka Machi, 2017
Taarifa ya Utekelezaji wa Bajeti ya SMZ kwa mwaka wa Fedha wa 2016/17 (iko kwenye hotuba ya Bajeti Kuu ya SMZ ya mwaka 2017/18 iliyotolewa barazani na Waziri wa Fedha wa Zanzibar) inaonyesha makusanyo ya SMZ mpaka Machi, 2017 yalikuwa ni shilingi 406.9 bilioni, kutoka vyanzo vifuatavyo; Ndani (389.6 bilioni), Nje (58.6 bilioni). Katika vyanzo vya ndani, Mapato ya Kodi yalikuwa ni shilingi 366.0 bilioni (makusanyo ya ZRB na TRA), na Mapato yasiyo ya Kodi (23.6 bilioni)
Taarifa hiyo inaonyesha pia kuwa jumla ya Matumizi halisi ya SMZ mpaka Machi, 2017 yalikuwa ni shilingi 424.8 bilioni, shilingi 378.3 zikitokana na mapato ya ndani, na shilingi 46.5 zikitokana na ruzuku, mikopo na michango ya Washirika wa Maendeleo.
3. Makusanyo ya TRA ya Zanzibar Hubaki kwa SMZ, Hayatokei Kwenye Hesabu za SMT
Kikawaida makusanyo ya TRA Zanzibar hubaki Zanzibar, hutuzwa kwenye akaunti za SMZ, na huhesabika kuwa ni mapato na makusanyo ya Zanzibar, Kamwe fedha hizi hazichanganywi na mapato ya Serikali ya Muungano. Makusanyo haya, pamoja na matumizi yake, hukaguliwa na Ofisi ya CAG Zanzibar. Hivyo basi, hesabu zake hazitarajiwi kutokea kwenye ripoti ya CAG iliyokabidhiwa bungeni.
Ndio maana taarifa ya utekelezaji wa bajeti ya Zanzibar ya mwaka 2016/17 imeeleza namna makusanyo husika ya TRA na ZRB yalivyofanyika na namna fedha hizo zilivyotumika katika miezi 9 ya mwaka wa fedha 2016/17. Fedha zote za TRA Zanzibar kwa miezi hiyo 9 zimekusanywa na kubaki chini ya SMZ, na kutumika na SMZ bila kupitia SMT.
Mpaka Machi, 2017, Fedha ambazo SMZ hawakuwa wamekusanya kutoka TRA Zanzibar ni mapato tarajiwa ya robo ya mwisho wa mwaka (Aprili - Juni, 2017) yaliyokadiriwa kufikia shilingi 52.8 bilioni.
4. PAYE za Watumishi wa SMT Walioko Zanzibar Hukusanywa na SMT kwa Niaba ya SMZ
Fedha pekee za mapato ya kikodi ambazo Serikali ya Muungano huzikusanya kwa niaba ya SMZ, ni fedha za makato ya Kodi (PAYE) za watumishi wa Serikali ya Muungano wanaofanyakazi Zanzibar, watumishi hawa ni kama Polisi, Wanajeshi nk. Fedha hizi hukusanywa kila mwezi na TRA makao makuu, hutunzwa kwenye akaunti ya hazina Benki Kuu ya Tanzania, na kisha hupelekwa hazina ya Zanzibar.
Fedha hizi hukusanywa kila mwezi, na zinapaswa kupelekwa Zanzibar kila mwezi ili kugharamia shughuli mbalimbali za SMZ. Kwa mwaka wa fedha wa 2016/17, matarajio ya makusanyo PAYE yalikuwa ni shilingi 21 bilioni. Kwa kuwa idadi ya watumishi hawa inafahamika, Wizara ya Fedha ya Zanzibar, wakati ikielezea utekelezaji wa Bajeti ya 2016/17, ilionyesha kuwa yalikusanywa yote kwa 100%.
5. Akaunti ya Zanzibar BOT Haionyeshi Uwepo 203.9 Bilioni
Fedha za Zanzibar kwenye akaunti zake Benki Kuu (BOT) zinaweza kuonekana kwa urahisi kwenye Hesabu za Benki Kuu. Hesabu za BOT kwa mwaka unaoishia Juni 30, 2017 hazionyeshi uwepo wala upitishwaji wa hizo shilingi 203.9 bilioni ambazo SMT wanadai kuikusanyia SMZ. Hata wakati wa kufunga hesabu za BOT kwa mwaka 2016/17 fedha pekee zilizokuwa kwenye akaunti hiyo zilikuwa ni shilingi Bilioni 14.
Serikali Ijibu Maswali Haya. Isituhadae!
Maelezo ya SMT bungeni ni kinyume na nyaraka za BOT, pamoja na taarifa za Wizara ya Fedha na Mipango ya Zanzibar. Ni vema sasa SMT ijibu chanzo cha mapato haya ya kikodi (203.9b) ni kipi? Kama fedha zilizokusanywa na TRA Zanzibar, zimeonywesha na SMZ kwenye BLW kuwa zimekusanywa, kubaki na kutumika Zanzibar, hizi SMT inazodai kuikusanyia Zanzibar na kukaa nazo kwa mwaka mzima ni zipi? Na ziko wapi? Fedha hizi zimekusanywa na kulipwa Zanzibar kupitia akaunti gani? Zanzibar wamepewa lini fedha hizi? Matumizi yake ni yapi kwa mujibu wa bajeti iliyopitishwa na BLZ?
Kwa taarifa ile ya Serikali Bungeni, mpaka Juni 30, 2017, ni wazi kuwa SMT bado ilikuwa imezishikilia fedha za SMZ, ambazo kikawaida hutolewa kila mwezi ili kuwezesha Zanzibar kujiendesha. Tukiamini kuwa huu ndio ukweli, na kuwa bunge halijadanganywa, basi ni dhahiri kuwa tunapaswa kuamini kuwa Serikali ya Zanzibar ilikuwa inajiendesha kwa MIUJIZA, ikikusanya mapato HEWA na kufanya matumizi ya KUFIKIRIKA ya mishahara, ruzuku, pensheni kwa wazee na miradi ya maendeleo.
Maana ni jambo lisiloweza kuingia akilini kuwa Fedha zote zinazokusanywa kwa niaba ya Zanzibar Katika mwaka 2016/17 hazikutolewa kwenda Zanzibar na kubakia Bara mpaka baada ya mwaka kuisha. Pia taarifa za mwenendo wa Akaunti za SMZ zilizoko BOT ni uthibitisho wa dhahiri kuwa hakukuwa na fedha za SMZ, shilingi 203.9 bilioni zilizoshikiliwa na SMT wakati au mara baada ya mwaka wa fedha wa 2016/17 kuisha.
Kama SMT wanadai kubaki na fedha hizi kwa  mwaka mzima wa fedha (2016/17), na kushindwa kuziwasilisha hesabu zake kwa CAG miezi mitatu baada ya mwaka wa fedha kufungwa (Septemba 2017), na hata kwenye Exit Meeting (Januari 2018), ni vema waonyeshe tu hata walikozitunza katika akaunti zao BOT.
Shilingi 1.5 trilioni ni karibu mara 2 ya bajeti yote ya Zanzibar, kupotea namna hii na maelezo ya kupotea kwake yawe ni uongo wa kuisingizia Zanzibar ni dharau kubwa kwa Zanzibar, ni kuidogosha Zanzibar, ni kitengeneza kero mpya ya muungano wetu kwa SMT kuitupia madudu yake SMZ, ni hadaa kwa umma, ni kutudharau Watanzania. Hatutakubali. Tutaendelea kuhoji ziliko shilingi 1.5 trilioni zetu mpaka tujue ziliko.
Mwisho, sisi ACT Wazalendo, tunaendelea kumsihi Spika wa Bunge aruhusu Ukaguzi Maalum wa matumizi ya Shilingi 1.5 trilioni kupitia Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali, PAC. Ni muhimu sana Bunge lichukue wajibu wake kwenye jambo hili linalohusisha matrilioni ya fedha za umma.
1.5trilioniZipoWapi?
Ado Shaibu
Katibu wa Itikadi, Mawasiliano ya Umma na Uenezi
ACT Wazalendo
Dar es Salaam
Aprili 24, 2017
Share This
Previous Post
Next Post

Pellentesque vitae lectus in mauris sollicitudin ornare sit amet eget ligula. Donec pharetra, arcu eu consectetur semper, est nulla sodales risus, vel efficitur orci justo quis tellus. Phasellus sit amet est pharetra

0 maoni: