![]() |
| Advertisement |
Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi amevitaka vyombo vya dola kufanya kazi kwa kuheshimiana katika kesi inayomkabili Harbinder Seth na James Rugemalira, akihoji sababu za Seth kutopelekwa katika matibabu kama ilivyoagizwa.
Leo Aprili 11, 2018 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, hakimu Shaidi amesema haipendezi kila mara amri za mahakama kutoheshimiwa na kusisitiza kuwa chombo hicho cha dola kinafanya kazi kwa mujibu wa sheria.
Hakimu Shaidi ametoa kauli hiyo baada ya wakili wa Serikali, Nassoro Katuga kueleza agizo lililotolewa na mahakama la kumpeleka Seth Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kwa matibabu halijatekelezwa na kwamba wanasubiri taarifa kutoka kwa mshtakiwa kuhusu daktari wake na kwamba sababu nyingine iliyowafanya washindwe kutekeleza agizo la mahakama kwa wakati ni mshtakiwa kuhamishwa kutoka gereza la Segerea kwenda gereza la Ukonga.
Hata hivyo Wakili wa utetezi, Hajra Mungula amepingaana na utetezi wa aakili Katuga na kudai kuwa mshtakiwa hajaongea chochote na kwamba wanashtushwa na maneno yaliyotolewa na upande wa mashtaka.
Mungula amedai kuwa agizo la mahakama wakati linatolewa Machi 28, 2018 tayari mshtakiwa huyo alikuwa amekwishapelekwa gereza la Ukonga na kuongeza kwamba hali ya Seth si nzuri na kwamba suala la afya si la mzaha “hatuwezi kuendelea na kesi mtu akiwa mgonjwa.”
Pamoja na hayo Wakili huyo amedai kuwa imekuwa ngumu kwenda kumuona gerezani Bw. Seth na hata kumpa dawa na kwamba hawajui upande wa mashtaka unadhamira gani huku akisisitiza kuwa haruhusiwi mtu yeyote kumuona hata mke wake wa ndoa na kuomba mahakama iliangalie hilo.
Seth na Rugemalira wanakabiliwa na mashtaka 12 ya uhujumu uchumi, utakatishaji fedha na kuisababishia Serikali hasara ya Dola za kimarekani 22, 198,544.60 (Sh309.5bilioni) katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Hakimu Shaidi ameahitisha kesi hiyo mpaka April 25 kwa ajili ya kutajwa.


0 maoni: