![]() |
| Advertisement |
Dodoma. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo ameliomba Bunge kuidhinisha Sh6.586 trilioni katika mwaka wa fedha 2018/19 huku akiainisha miradi mikubwa itakayofanywa katika jiji la Dar es Salaam ya kuboresha mradi wa usafiri wa mabasi yaendayo haraka.
Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake bungeni jana, Jafo alisema katika mwaka wa fedha 2018/19 Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam (Dart) utatekeleza awamu ya pili ya ujenzi wa miundombinu wa mabasi kuanzia Desemba.
Alisema ujenzi huo utakahusisha barabara za Kilwa, Kawawa, Sokoine, Gerezani, Bandari na Changombe zenye urefu wa kilomita 20.3.
“Ujenzi huu umepangwa kuanza Desemba mwaka huu baada ya kumpata mkandarasi. Mradi huu utatekelezwa kupitia mkopo wa Dola milioni 141.71 za Marekani kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika,” alisema.
Alisema pia kutakuwa na awamu ya tatu ya ujenzi wa miundombinu ya Dart utakaohusisha barabara za Nyerere, Uhuru, Bibi Titi, Azikiwe, Shaurimoyo, Lindi na Maktaba zenye urefu wa kilomita 23.6.
Alisema kazi hiyo itafanyika kwa mkopo wa Benki ya Dunia wa Dola milioni 148.2 za Marekani na kazi ya ujenzi huo pia imepangwa kuanza Desemba.
Waziri Jafo alisema kazi ya usanifu wa awamu ya nne ya ujenzi wa miundombinu ya Dart kwa mkopo wa Dola milioni 97.9 za Marekani kutoka Benki ya Dunia itaanza katika barabara za Sam Nujoma, Bagamoyo, Bibi Titi na Ali Hassan Mwinyi zenye urefu wa kilomita 25.9.
Pia, Dart itatekeleza mpango kazi wa fidia ya makazi kwa waathirika wa mradi wa awamu ya pili na tatu ikiwa ni pamoja na kulipa fidia kwa ajili ya miradi ya awamu ya pili, tatu na nne.
Bonde la Msimbazi
Pia, Jafo aligusia suala la Bonde la Msimbazi jijini Dar es Salaam akisema kupitia programu ya kuendeleza miundombinu ya jiji hilo Serikali inaendelea na usanifu wa mradi wa bonde hilo unaofanywa na kampuni mbili za COWI Tanzania Limited na Ecorys ya Uholanzi ili kumpata mkandarasi wa kujenga na kuboresha miundombinu.
“Kazi ya usanifu imepangwa kukamilika Juni mwaka huu. Mradi huu utatekelezwa kwa mkopo wa Dola milioni 20 za Marekani kutoka Shirika la Maendeleo Uingereza (DFID) ikiwa ni mkakati wa kupunguza athari za mazingira na mafuriko katika bonde hilo.
Watumishi hewa waiathiri LAPF
Mbali na ujenzi wa barabara hizo, Jafo alisema katika mwaka wa fedha 2017/18, Mfuko wa Pensheni wa Serikali za Mitaa (LAPF) ulipanga kukusanya Sh611.67 bilioni.
Hata hivyo, ulilazimika kufanya marekebisho ya makisio hayo kwa miezi sita kuwa Sh543.34 bilioni kutokana na kuondolewa kwa watumishi wasio na sifa katika sekta ya umma hivyo kiasi kilichopungua ni Sh68.33 bilioni.
Waziri Mkuchika
Sambamba na Waziri Jafo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika aliwasilisha bajeti yake na kueleza kuwa katika mwaka wa fedha 2018/19, Bodi ya Utumishi wa Mishahara na Maslahi katika Utumishi wa Umma, itafanya utafiti wa hali ya masilahi.
Alisema utafiti huo utahusisha mifumo ya kupima utendaji kazi ili kushauri namna bora ya kutoa motisha kwa kuzingatia utendaji ili kuongeza ufanisi katika kuhudumia wananchi.
Alisema pia bodi hiyo itaandaa taarifa nne za gharama za maisha kama msingi wa kukadiria kima cha chini cha mshahara wenye staha na taarifa hizo zitawezesha kushauri kuhusu mshahara wa chini unaoendana na gharama halisi za maisha.
Alisema pia bodi hiyo itatekeleza mapendekezo yanayotokana na tathmini ya kazi na uhuishaji wa madaraja katika utumishi wa umma.
Mkuchika ameomba Bunge liidhinishe Sh669.09 bilioni kwa ajili ya mafungu ya Ofisi ya Rais Ikulu, Sekretarieti ya Baraza la Mawaziri na Menejimenti ya Utumishi wa Umma.
Mafungu mengine ni ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Tume ya Utumishi wa Umma, Bodi ya Mishahara na Masilahi katika Utumishi wa Umma na Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa.


0 maoni: