Alhamisi, 12 Aprili 2018

Mawaziri watano kujibu hoja za CAG

ad300
Advertisement

Dodoma. Mawaziri watano leo watakuwa na kazi ya kujibu baadhi ya hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kutokana na kuguswa katika taarifa aliyoiwasilisha bungeni Jumatano Aprili 10.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe aliwaambia waandishi wa habari jana mjini hapa kuwa leo saa 5:00 asubuhi katika Ukumbi wa Idara ya Habari uliopo bungeni ataongoza mawaziri wenzake kujibu hoja hizo.

Profesa Mussa Assad aliwasilisha bungeni ripoti yake jana na inaonekana kuwagusa kwa karibu mawaziri watano baada ya wizara zao kutajwa katika taarifa hiyo ikionyesha upungufu katika baadhi ya maeneo, aliyosema yanajenga shaka.

Taarifa hiyo imeacha maswali yatakayohitaji majibu kutoka kwa mawaziri hao, ingawa waziri wa Tamisemi atatakiwa kutolea ufafanuzi hoja nyingi zaidi, ikiwemo uwajibikaji wa watumishi waliosababisha hasara mbalimbali.

Hoja nyingine ni kushindwa kwa miradi ya maendeleo baada ya ripoti hiyo kuonyesha kuwa makusanyo yalifikia asilimia 94 ya malengo, lakini fedha zilizokwenda katika miradi ni asilimia 51 tu na kuathiri miradi mingi.

Profesa Assad alikataa kujibu swali kuhusu fedha zilikokwenda, akitaka iulizwe Serikali.

“Tulitaka kujibu mambo hayo leo (jana), lakini tumeona mtakuwa na mambo mengi kwa wakati mmoja, hivyo tumeamua kuyajibu kwa pamoja kesho (leo),” alisema Dk Mwakyembe.

“Na mimi nitawaongoza wenzangu kuja kujibu hoja hizo hapa hapa ili msikie nasi upande wetu.”

Mapema jana kabla ya CAG kusoma ripoti yake mbele ya waandishi wa habari, Idara ya Habari ilisema kuwa mawaziri wawili, Dk Philip Mpango (Fedha) na Seleman Jafo (Tamisemi) wangekutana na wanahabari kujibu baadhi ya hoja za ukaguzi.

Mara baada ya CAG kumaliza taarifa yake, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage na Dk Mwakyembe walifika mbele ya wanahabari na kutaka kuzungumza, lakini wakakubaliana kusubiri wenzao ili jambo hilo lifanyike kwa pamoja leo.

Kwenye taarifa yake, CAG, aligusia upungufu katika taasisi za Serikali, upungufu katika fedha za maendeleo kwa serikali za mitaa, misamaha mingi ya tozo ikiwemo ushuru wa mafuta unaotumika kwenye migodi, deni kubwa la matibabu nje ya nchi na ukaguzi katika Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).

Maeneo mengine yaliyoonyesha mashaka katika taarifa hiyo ni Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa Taifa (NSSF), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Bandari (TPA) na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) na taasisi nyingine.

Profesa Assad alisema taasisi hizo zimetumia fedha nyingi kufanya manunuzi ambayo hayana viambatanisho, hivyo kutia hofu kubwa.

Pia ametilia shaka dhidi ya Shirika Hodhi la Reli (Rahco), Bohari ya Taifa ya Dawa (MSD), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Mfuko wa Maendeleo wa Korosho (CIDTF).

Profesa Assad alisema Taifa limepoteza mabilioni ya fedha ambazo zingeweza kutumika katika miradi mingine yenye tija kwa wananchi lakini bado kuna maeneo yanashangaza kutokuchukua hatua na kufanya marekebisho.

Wizara ya Afya yaguswa

Pia Wizara ya Afya imetajwa kuwa na ongezeko la deni la matibabu ya nje la Sh17.13 bilioni katika Hospitali ya India, deni hilo lilikuwa Sh28.60 bilioni Juni 30, mwaka jana, lakini lilifikia Sh45.73 bilioni, Desemba 31, mwaka huo.

“Ongezeko hili la asilimia 60.71 kwa kipindi kifupi ni jambo linalohitaji Serikali kulifuatilia kwa makini ili kupunguza mzigo wa madeni na kuhakikisha kuwa hospitali zinalipwa kwa wakati,” alisema Assad.

Wizara ya Fedha

Taarifa fupi aliyoitoa kwa wanahabari inaonyesha kuigusa kwa karibu Wizara ya Fedha katika maeneo mengi kutokana na upungufu mkubwa wa usimamizi wa matumizi ya fedha kwa mwaka 2016/17 zikiwemo Sh332.86 bilioni zilizotumika vibaya katika ubalozi wa Tanzania nchini Msumbiji.

Kesi za kodi zilizochukua muda mrefu katika mahakama za rufaa zimesababisha upotevu wa Sh4.44 trilioni na amesema TRA imekuwa na mashauri mengi, lakini yamekwama kwa muda mrefu bila sababu za msingi.

Kingine ni pingamizi za TRA zinazofikia Sh738.61 bilioni, lakini hazijashughulikiwa, huku mamlaka ikipokea pingamizi za kodi zinazofikia Sh296.09 bilioni bila kukusanya amana ya pingamizi na kupata kibali cha amana kutoka kwa kamishina kinyume cha matakwa ya kisheria.

Wizara ya Habari

Waziri wa Habari atatakiwa kutolewa ufafanuzi wa mkataba kati ya TBC na Star Times ambavyo viliainishwa kuwa na upungufu mkubwa wa sheria na hivyo kuwepo na hofu ya upande mmoja kuumizwa.

Wizara ya Viwanda

Pia CAG amesema sera ya viwanda inaweza isifanikiwe kabisa nchini kwani ofisi yake ilibaini upungufu katika utoaji wa huduma za mafunzo, masoko, mitaji na teknolojia.

“Hivyo kuna hatari kubwa ya kutofikia kwa sera ya viwanda Tanzania iwapo sekta ya wajasiriamali wadogo na wa kati haitapewa kipaumbele cha kutosha,” alisema Profesa Assad.

Katika hatua nyingine CAG amelalamikia mashirika na taasisi nyingi kuongozwa na bodi zilizomaliza muda wake na ama kutokuwepo kabisa bodi, jambo linalozorotesha ufanisi wa kazi katika maeneo hayo na kuomba mamlaka husika kuwa na tahadhari katika maeneo hayo.

Hata hivyo, baada ya kauli hiyo kutolewa, saa tatu baadaye Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Iklulu ilitoa taarifa kuwa ya uteuzi wa Profesa Isaya Jairo kuwa mwenyekiti mpya wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA) .

Taarifa hiyo iliyotolewa na Gerson Msigwa inasema uteuzi huo ulianza jana.

Share This
Previous Post
Next Post

Pellentesque vitae lectus in mauris sollicitudin ornare sit amet eget ligula. Donec pharetra, arcu eu consectetur semper, est nulla sodales risus, vel efficitur orci justo quis tellus. Phasellus sit amet est pharetra

0 maoni: